Kuhusu Kamata Fursa

Jukwaa la kamata fursa ni kurunzi inayokwenda kutoa nuru kati kati ya giza totoro. Msukumo na maono ya uanzishwaji wa jukwaa la kamata fursa umejikita zaidi katika msemo wa wahenga kuwa usilolijua ni sawa na usiku wa giza. Takwimu za kipato duni, hasa kwa vijana hazipaswi kuendelea kufumbiwa macho. Hivyo basi, kutokana na dhamiira ya dhati ya kuinua hali ya maisha, jukwaa la kamata fursa limebuniwa ili kila Mtanzania kokote kule aliko aweze kubaini hazina ya mianya ya mafanikio iliyoko sehemu mbali mbali nchini kupitia sekta za huduma, viwanda, miundombinu, biashara , mifugo, kilimo na nyinginezo nyingi.

Jukwaa la kamata fursa limejielekeza zaidi katika kuondoa vikwazo na urasimu wa taarifa na maarifa kwa wananchi wa kawaida hususani vijana kwa lengo la kurahisisha uelewa, upatikanaji wa taarifa sahihi na kufanya maamuzi ya kufaidika na fursa kwa wakati. Licha ya tatizo la usambazaji, uzoefu unaoyonyesha kwamba machapisho mengi yamekuwa yakihifadhi maarifa kwa lugha ngumu na wakati mwingine kuwabagua wajasiriamali kwa vigezo vya elimu , uwezo wa kiuchumi na maeneo ya kijiografia. Kupitia jukwaa hili na ubunifu wa hali ya juu, taarifa zinachujwa, kutafsiriwa, kurahisishwa na kutangazwa kwa kasi ili kuweza kuwavutia na kuwafikia watu wengi wa kada mbali mbali mijini na vijijini.

Kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano, jukwaa la kamata fursa limedhamiria kuondoa vikwazo na kuwaunganisha Watanzania moja kwa moja na masoko kwa kutangaza fursa za ndani na nje ya nchi, kutoa taarifa na maarifa stahiki kuhusu mianya ya mafanikio na kupanua wigo mpana wa ubunifu katika kutatua changamoto za kimaendeleo. Jukwaa la kamata fursa linapanua wigo wa ushiriki wa makundi yote katika uzalishaji ili kuharakisha kufikiwa kwa lengo la UCHUMI WA KATI nchini Tanzania.